Jumapili, 13 Julai 2014

Wiki iliyopita niliwasilisha makala


Wiki iliyopita niliwasilisha makala haya kuhusu “ongezeko la imani za uchawi makanisa Tanzania” na kutoa takwimu za tafiti zilizofanyika ambazo zimeiweka Tanzania kuongoza kimataifa kwa uchawi katika Bara la Afrika. Takwimu za kutisha zilidai 93% ya watanzania wanaamini katika uchawi na kujihusisha na vitendo vya ushirikina na uchawi. Aidha niliweka bayana Madhumuni ya makala haya kuwa ni kuelimisha, kutahadharisha na kuonya kanisa kuonesha mamlaka ya Kristo aliyoliachia; na sio kutangaza imani potofu inayodai kwamba wachawi wafreemasons ndio wanaofanikiwa kiuchumi. Leo ninaendelea na uchambuzi wa hoja hii nyeti:

Marejeo ya athari za imani za uchawi makanisa

Askofu Sylvester Gamanywa
Madai yaliyotawala ndani ya baadhi ya makanisa ni “tuhuma-shirikina” zinazodai kwamba baadhi ya watu wanaoonekana kufanikiwa kiuchumi “makanisani”; hata kama ni wacha-Mungu lazima wamepata utajiri kwa za uchawi wa freemason. Hii ni pamoja na watumishi wa Injili ambao wanatokea kuwa na wafuasi wengi katika mikutano yao, au ibada zao, nao hutuhumiwa kutumia “ndumba za freemason”

Aidha, nidokeza bayana kwamba, kuongezeka kwa kasi ya hizi “tuhuma-shirikina” tayari kumekuwa “kichocheo” kwa baadhi ya waamini wenye “imani dhaifu” kujikuta wanashawiki kuwasaka akinafreemason wakitaka kujua ni akina nani, wako wapi ili wajiunge na kuupata utajiri kama unavyotangazwa “makanisani”!

Athari nyingine mbaya zaidi itokanayo na “tuhuma-shirikina” ni kufuga tabia ya uvivu makanisani ambapo waamini hudhoofika kifikra na bidii ya kufanya kazi ambayo ndiyo njia muafaka ya kiuchumi; na kujengewa tabia ya “utegemezi wa maombezi ya kuvunja laana” kama njia peke ya kufanikiwa kiuchumi! Ile mantiki nzima ya “maombezi” imepoteza mwelekeo wake wa Kibiblia!

Hata hivyo, nilitahadharisha mapema kwamba sipingi wala sikatai kuwepo kwa uchawi na wachawi. Pia siko kinyume na huduma halisi za kukemea pepo wachafu na roho za mizimu ya uchawi. Nilikiri na kuthibitisha na kutambua utekelezaji wa agizo kuu la Yesu Kristo aliposema “kwa jina langu watatoa pepo”! Ninachopinga ni hali ya kupoteza mwelekeo ambapo “kutoa pepo” kumemezwa kiushirikina na “kupunga pepo”!

Kama nilivyobanisha kuhusu madhumuni ya makala, na bado nasisitiza kwamba, nia ni kuelimisha, kutahadharisha na kulionya kanisa kwa upendo na upole, lirudi kwenye wito wake asilia wa kuidhihirisha mamlaka ya Kristo lilioachiwa; badala ya kutangaza na kutukuza nguvu za uchawi wa freemason!

Historia ya Nimrodi mwasisi wa Uchawi

Nimrodi ni mtoto wa Kushi, mjukuu wa Hamu ambaye ni mwana wa Nuhu! Imeandikwa Nimrodi alikuwa hodari wa kuwinda wanyama mbele za BWANA. Yeye ndiye mwasisi wa ufalme wa Babeli pamoja na “tawala za kifalme” za Ereku, na Akadi, na Kalne katika nchi ya Shinari. Ni huko huko katika nchi ya Shinari Biblia imeandika:

Ikawa watu waliposafiri pande za mashariki waliona nchi tambarare katika nchi ya Shinari; wakakaa huko. Wakaambiana, haya, na tufanye matofari tukayachome moto. Walikuwa na matofari badala ya chokaa. Wakasema, haya, na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni, tujifanyie jina; ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote.” (Mw.11:2-4)

Kwa kupitia maandiko haya, inasadikiwa kuwa ndio mwanzo wa imani za uchawi ambazo mwasisi wake ni Nimrodi. Wengine wanatafsiri kwamba, kile ambacho Nimrodi alikuwa anakijenga sio mnara wa kawaida ambao alikusudia ufike mbinguni, bali ulikuwa alikuwa akiongozwa na nguvu za uchawi katika ujenzi huo, na ndio maana ilibidi Mungu mwenyewe kuingilia kati ili kusitisha uchawi huo:

BWANA akashuka ili auone mji na mnara waliokuwa wakiujenga wanadamu. BWANA akasema, tazama, watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya, wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya. Haya, na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao. Basi BWANA akawatawanya kutoka huko waende usoni pa nchi yote; wakaacha kuujenga ule mji. Kwa sababu hiyo jina lake likaitwa Babeli; maana hapo ndipo BWANA alipoichafua lugha ya dunia yote; na kutoka huko BWANA akawatawanya waende usoni pa nchi yote.” (Mw.11:5-9)



Mfano wa mnara wa Babeli

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni