Jumapili, 13 Julai 2014

KWA TAARIFA YAKO HII NDIO SIRI YA MARTHA MWAIPAJA KUIMBA NYIMBO ZA KUTIA MOYO

Haya msomaji wetu wa Gospel Kitaa karibu katika kipengele chetu cha ''KWA TAARIFA YAKO'' ambacho kinakujia kila siku za alhamisi ndani ya GK kikiwa na lengo la kukupatia habari ambayo iliwahi kutukia lakini yawezekana huijui pia yawezekana ilitukia ukawa unaijua lakini GK ikawa imesahau mahali au kuna sehemu haina usahihi utapata fursa ya kusahihisha kwa kuweka comment yako chini kabisa kwenye habari husika. Karibu.


KWA TAARIFA YAKO hii leo ina mhusu mwimbaji nyota ambaye ana album mbili tangu aanze huduma ya uimbaji na album zote mbili zimekuwa zikipendwa na watu wengi, huyu si mwingine bali ni Martha Mwaipaja au mwite mama mchungaji John Said. Mwimbaji huyu ana mengi na mazito aliyopitia katika utoto wake mpaka kufikia hapo alipo. Martha amekuwa akiimba nyimbo za kutia moyo sana kuliko za shangwe kama baadhi ya waimbaji wengine wanavyofanya, nyimbo zake nyingi ni za kutia moyo hasa kwa watu wanaopitia magumu mbalimbali kama ukisikiliza wimbo wake wa "Tusikate tamaa" katika album yake ya "Kwa msaada wa Mungu tunashinda" vivyo hivyo ukisikiliza album yake ya pili kama wimbo uliobeba album "Ombi langu kwa Mungu".

KWA TAARIFA YAKO sasa kama ulikuwa hujui ni kwamba kutokana na maisha aliyoishi Martha ya kunyanyasika yeye, mama yake na wadogo zake kukosa hela ya kula,kukosa pesa ya kwenda shule hii ni baada ya baba yake kufariki dunia pia mama yake mzazi kukataa kurithiwa na mwanaume mwingine (mila za zamani za Kinyakyusa au labda wengine bado wanaziendeleza) kitendo hicho cha kukataa kiliwafanya wapate matatizo zaidi likiwemo nililolitaja mwanzoni lakukosa pesa ya kula kuna wakati walifanyiwa vituko vingi ili mradi tu wahame kwenye nyumba waliyokuwa wakikaa ilifikia kuna wakati walilala hata nje. Kwahiyo kutokana na shida zote hizi alizopitia hadi kufikia hapa alipo amekuwa na mzigo mzito kwa watoto waliofiwa na wazazi wao au wanaoishi katika mazingira magumu na watu wengine wanaopitia shida alizopitia.

Akiwa katika kanisa la Ufufuo na Uzima ambalo ndio kanisa lake alikotoka baada ya kuolewa na mchungaji John Said aliweza kuandaa album ya kwanza akitanguliza wimbo wa "Tusikate tamaa" wimbo ambao ulianza kupigwa kupitia kipindi cha Ipo njia na Njoo tusemezane vyote vya WAPO Radio FM mtangazaji aliyeutambulisha wimbo huo akiwa Silas Mbise ambaye naye alivutiwa sana na wimbo huo kiasi cha kuupiga kila alipoingia studio na ndani ya mwezi mmoja tangu aanze kuupiga mfululizo ukashika masikio na myoyoni mwa watu kisha Martha akamaliza album yake ambayo imefanyika baraka sana kwa watu wengi kutokana na jumbe zilizojaa katika nyimbo hizo.

KWA TAARIFA YAKO baada ya kuolewa kwake Martha Mwaipaja na mchungaji kuna watu walidhani kwamba itakuwa ndio mwisho wayeye kuimba ama kutoonekana katika majukwaa ya uimbaji la hasha Martha amekuwa akipewa sapoti ya kutosha na mumewe katika uimbaji kama ilivyoshuhudiwa katika uzinduzi wa album yake ya pili katika viwanja vya Mwalimu JK Nyerere ambako mumewe alikuwa sambamba lakini kama haitoshi unaweza kumuona mumewe Martha ndani ya video yake ya Ombi langu kwa Mungu. Ambapo kupitia maswali aliyoulizwa na wasomaji wa GK kuhusu anaonaje maisha yake kama mke wa mchungaji na zamani kabla hajaolewa, Martha amesema anaona utulivu ambao ameupata na anauona katika ufahamu wake sasa hivi tofauti na zamani lakini pia ndoa yake anaona kama daraja la kumfikisha mbali zaidi kihuduma. KWA TAARIFA YAKO ombi lake kuu Martha ni kuona Mungu anawakumbuka watoto wanaopata shida na matatizo mbalimbali na kwasasa lengo lake ni kufungua shule itakayowasomesha watoto hao na pia kufanya misaada mbalimbali.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni